Watanzania wamekumbushwa kutendeana mema bila kubaguana ili kuimarisha amani na upendo kwa binadamu wote na ustawi wa jamii yenye kutanguliza uzalendo na maslahi ya Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mhashamu Askofu Lazarus Msimbe wa Jimbo Katoliki Morogoro wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Ijumaa Kuu katika Kanisa Kuu la Katoliki la Kiaskofu la Mtakatifu Patrick mkoani Morogoro
Akiongea na waumini walioshiriki ibada hiyo Askofu Msimbe amesema katika jamii kumekuwa na watu wasiotenda haki kwa makusudi na kuwaonea wengine kama alivyofanya Pilato wakati Yesu Kristo akisulubiwa bila hatia.
Ameongeza kuwa kupitia ibada kama hiyo Watanzania wanakumbushwa kutenda haki kwa jamii ili kauondoa migawanyiko kati ya wenye kuonewa na wenye mamlaka na maamuzi katika maeneo mbalimbali ikiwepo uongozi kwa ngazi za familia na makundi mengine.
“Nawasihi ndugu Watanzania na wanadamu wote tusiwatenge au kuwanyanyasa watu kwa sababu ya dini zao na makabila yao, bali tuishi kwa kupendana kwa umoja wetu ili kuwa na jamii yenye furaha na amani wakati wote katika Taifa letu,” amesisitiza Askofu Msimbe
Ibada hiyo imefanyika kanisani hapo ikiwa ni maadhimisho ya siku ya Ijumaa Kuu ambapo ulimwenguni kote Wakristo wakidhimisha kipindi cha Kwaresima ikiwa ni kukumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo na kufunga kwaajili ya kufanya toba.