Watanzania waadhimisha miaka 58 ya Muungano

0
333

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulioasisiwa Aprili 26 mwaka 1964.

Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muungano wa mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,  ambayo yaliingia mkataba wa muungano mwaka huo wa 1964 na kuanzishwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa ZanzibarHayati Sheikh Abeid Amani Karume Aprili 22 mwaka  1964 huko Zanzibar na baadaye mkataba huo ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi.

Aprili  27 mwaka huo huo wa 1964, Viongozi hao walikutana katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam na kubadilishana Hati za Muungano na Oktoba 28 mwaka huo huo kulifanyika mabadiliko ya jina ambapo jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lilibadilishwa na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sherehe za miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zinafanyika kitaifa mkoani Dodoma.

Kwa upande wa mikoa na wilaya, Serikali imewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini kote kuandaa shughuli za kufanya kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya kusherehekea miaka.58 ya Muungano

Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano ni Uwajibikaji na Uongozi Bora, Tushiriki Sensa ya Watu na Anwani ya Makazi kwa maendeleo yetu.