Watanzania waadhimisha miaka 57 ya Uhuru

0
1862

Watanzania leo wanaadhimisha miaka 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Uhuru uliopatikana Disemba Tisa mwaka 1961.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Rais  John Magufuli kwa mujibu wa Mamlaka aliyopewa,  ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477,  ambapo 1,176 kati yao wanatoka hii leo.

Msamaha huo unawahusu wafungwa wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito, na waliongia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

Halikadhalika, Rais Magufuli ameamua wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye Kifungu cha  49 (1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58.

Hata hivyo, msamaha huo hauwahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo za kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu, makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka, kulawiti na makosa  kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo wa Rais ni wale wa makosa ya uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, walioingia gerezani baada ya Disemba Mosi mwaka huu  au waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.