Watalii wavutiwa na Hifadhi ya Taifa Ruaha

0
278

Hifadhi ya Taifa Ruaha imeendelea kuwa kivutio cha Watalii wa ndani na nje ya nchi kutokana na vivutio vya kila aina hususani makundi ya Simba katika familia moja zaidi ya simba 40, utalii wa usiku na mchana na utalii wa miguu, hali inayomfanya Mtalii kukaa siku zaidi ya moja katika hifadhi hiyo.

Akieleza namna alivyofurahia Utalii ndani ya hifadhi hiyo, Mtalii Ines Richard kutoka Ufaransa amesema imekuwa ni zaidi ya matarajio kwa kuwa licha ya kuona makundi makubwa ya Simba, pia ameona wanyama wakubwa na wadogo, ndege aina zaidi ya 570 na mimea ya kila aina.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha Kamishna Msaidizi Mwandamizi Godwell Ole Meng’ataki ameeleza kuwa hifadhi hiyo imekuwa ikitembelewa na watalii wengi kutokana na utajiri wa vivutio kwenye hifadhi, malazi, vyakula vya bei rafiki na uvuvi wa Kitalii.

Ameongeza kuwa hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa nchini, imekuwa kivutio kikubwa kutokana na kuwa na miundombinu mizuri hasa barabara kupitia mradi wa Kukuza na Kuendeleza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).

Kupitia mradi huo hifadhi hiyo inatekeleza ujenzi wa kiwanja cha ndege, barabara ndani ya hifadhi, uchimbaji wa mabwawa 32 kwa ajili ya wanyama, ujenzi wa sehemu za malazi, kituo cha utafiti pamoja na sehemu Kwa ajili ya ulinzi wa maliasili.