Watalii waongezeka Hifadhi ya Mikumi

0
318

Idadi ya wageni wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Mikumi mkoani Morogoro imeongezeka maradufu hadi kufikia wageni 3,000 kwa mwezi katika siku za hivi karibuni.

Akizungumza na TBC, Afisa Uhifadhi, Daud Gordon amesema wageni wanaotembelea hifadhi hiyo kwa siku wameongezena na kufikia wageni 140 kutokana na kupungua kwa visa vya COVID19, kutoka wageni 9 kwa siku.

Mbali na wageni kutoka ndani ya nchi, amesema kuwa “kitakwimu wageni wanaotembelea hifadhi hii zaidi ni kutoka Taifa la Marekani ikifuatiwa na Bara la Ulaya hususani Urusi, huku Asia ikiongozwa na Uchina.”

Afisa huyo amebainisha pia kuwa Mikumi ni moja ya hifadhi zinazofikika kiurahisi kutokana na barabara kuu inavyokwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani kupita katikati ya hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Mikumi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,230 ni ya nne kwa ukubwa nchini Tanzania ikitanguliwa na hifadhi ya Nyerere, Ruaha na Serengeti. Ni nyumbani kwa wanyama mbalimbali wakiwemo Simba, Tembo, Nyati, Nungunungu, Pundamilia, Nyumbu, Kiboko, Mamba, Swala, Pofu na Mbwa mwitu.

Upekee mwingine wa hifadhi hiyo ni kuwa inaweza kutembelewa kipindi chochote cha mwaka.