Wakati mikakati ya kukabiliana na virusi vya corona ikiendelea kutekelezwa nchini Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amewataka wakazi wote wa mkoa huo ambao hawana ulazima wa kutoka majumbani mwao wabaki nyumbani ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.
Paul Makonda ameyasema hayo leo huku akibainisha kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaokiuka agizo hilo, ikiwa ni pamoja na kupewa adhabu ya kufanya shughuli za kijamii.
Aidha, baada ya kutoa agizo hilo, amewaelekeza wafanyabiashara mbalimbali kuendelea na biashara zao kama kawaida, huku wakichukua tahadhari dhidi ya virusi hivyo.
Hadi Aprili 5 mwaka huu, jumla ya visa 22 vya maambukizi ya corona vimerekodiwa nchini Tanzania, huku waliopona wakiwa ni watatu na mmoja akifariki.