Wataalamu watakiwa kubidhaisha Kiswahili

0
143

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameziagiza wizara na taasisi zinazohusika na maendeleo ya lugha ya Kiswahili kuwatumia wataalamu wa lugha hiyo waliopo nchini kukitangaza na kukibidhaisha kiswahili ili kitumike kama lugha ya ukombozi na kusaidia kuleta umajumui wa Afrika.

Pia ametoa wito kwa balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha zinaendeleza jitihada za kukuza na kufundisha Kiswahili katika ofisi za ubalozi na kuwashirikisha wadau wengine kama Diaspora na asasi nyingine zenye nia ya kukuza na kuendeleza Kiswahili.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022, iliyofanyika mkoani Dar es Salaam. 

Tuzo hizo zinadhaminiwa na kampuni ya mabati ya ALAF Limited – Tanzania ikishirikiana na kampuni ya Mabati Rolling Mills ya Kenya, chini ya uratibu wa Chuo Kikuu cha Cornell cha nchini Marekani.

“Muda mrefu imekuwa ikizoeleka kwamba lugha ya kiswahili inatumika katika masuala ya kitaaluma, lugha hii kwa sasa imeshavuka mawanda ya kitaaluma na inatumika katika nyanja za uchumi na biashara. Kwa kuzingatia ukweli huo leo tunashuhudia kwa macho yetu kampuni ya ALAF ikitoa tuzo na ufadhili wa wanafunzi wanaosomea shahada ya umahiri katika Kiswahili.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Amewasisitiza wataalamu wa kiswahili kuhakikisha wanaweka mikakati thabiti ya kupenyeza lugha ya kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandika kamusi na vitabu vitakavyowasaidia watu kujifunza lugha hiyo adhimu.