Wasomi waelezea msimamo wa Marekani dhidi ya ICC

0
1076

Wasomi mbalimbali nchini wamepokea kwa mtazamo tofauti hatua ya Marekani ya kutishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC endapo itawashitaki askari wake wanaodaiwa kufanya vitendo vya uhalifu nchini Afghanstan.

Miongoni wa wasomi hao ni Profesa wa sheria  kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Chris Peter Maina na mhadhiri wa chuo cha Diplomasia, – Abbas Mwalimu.

Profesa Maina ambaye amekuwa katika kamisheni mbalimbali za sheria za kimataifa amesema kuwa haoni nguvu yoyote ya Marekani katika kuathiri utendaji kazi wa ICC.

Naye Abbas Mwalimu ameukosoa uamuzi huo wa Marekani na kusema kuwa kuna umuhimu kwa mahakama hiyo ikaangalia upya hasa katika kipindi hiki ambacho haiungwi mkono na mataifa mengi hasa yale makubwa.

Hivi karibuni Marekani ambayo ni moja ya nchi ambazo haiiungi mkono mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu imetishia kuweka vikwazo dhidi ya mahakama hiyo endapo itaendelea na mikakati yake ya kuwashtaki raia wa nchi hiyo.

Mshauri wa masuala ya usalama ya kitaifa wa Marekani, -John Bolton amedai kuwa ICC  sio halali na kuapa kuwa nchi hiyo itafanya kila liwezekanalo kuwalinda raia wake.

Mahakama hiyo  ya Kimataifa ya Uhalifu  ambayo makao makuu yake yapo The Hague nchini Uholanzi, kwa sasa inafanya tathmini ili kuwafungulia mashtaka askari wa Marekani kwa madai ya kuwatesa wafungwa nchini Afghanistan.