Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mwananchi yeyote ambaye hatakabidhi silaha yake anayoimiliki isivyo halali hatasita kuchukuliwa hatua za kisheria.
Babu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kuongeza kuwa kipindi cha miezi miwili iliyotolewa kuanzia Septemba Mosi hadi Oktoba 30, 2022 inatosha kwa mwananchi awe ameshawasilisha silaha hiyo.
“Ndugu wanahabari natoa rai kwa watanzania hasa wa mkoa wa Kilimanjaro kutumia vizuri msamaha huu uliotolewa na serikali ili wasalimishe silaha hizo walizonazo kwani baada ya muda huo kupita Jeshi la Polisi litafanya msako mkubwa na yoyote atakayebainika kuwa na silaha hiyo atachukuliwa hatua kali za kisheria” amesema Babu
Babu amewataka pia viongozi wa dini kutumia makanisa na misikiti kupitia kamati za amani ngazi ya mkoa, wilaya na kata kutoa elimu kwa waumini wao juu ya kusalimishwa kwa silaha hizo.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro Saimon Maigwa amesema tayari wameshaanza kupokea baadhi ya silaha kutoka kwa wanaomiliki kinyume na taratibu ambapo amewatoa hofu kwamba hakuna hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi ya muwasilishaji.