Mama Samia Suluhu Hassan alizaliwa Januari 27 mwaka 1960 huko visiwani Zanzibar.
Alipata elimu ya msingi katika shule za msingi za Chawaka huko Unguja, Ziwani huko Pemba na Mahonda iliyopo Unguja kati ya mwaka 1966 na 1972.
Alisoma katika shule ya Sekondari Ngambo iliyopo Unguja kuanzia mwaka 1973 hadi 1975 na baadaye katika shule ya sekondari Lumumba iliyopo mjini Unguja mnamo mwaka1976 na kuhitimu mwaka 1977.
Mama Samia Suluhu Hassan aliajiriwa kuwa Karani katika Wizara ya Mipango na Maendeleo kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na akapanda ngazi hadi kuwa afisa wa mipango Serikalini kati ya mwaka na 1987 na 1988.
Aliendelea na safari yake ya kujiendeleza kielimu kwa kusoma kozi mbalimbali, ambapo mwaka 1986, alihitimu katika Taasisi ya Usimamizi wa Maendeleo ambayo kwa sasa kinaitwa Chuo Kikuu cha Mzumbe na kutunukiwa Stashahada ya juu katika Uongozi na Utawala wa Umma.
Baada ya kuhitimu, aliajiriwa kwenye mradi uliofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) .
Kati ya mwaka 1992 na 1994, Mama Samia Suluhu Hassan alisoma katika Chuo Kikuu cha Manchester huko Uingereza na kuhitimu Stashahada ya Uzamili katika uchumi.
Mwaka 2015 alipata Shahada za Uzamili katika Maendeleo ya Uchumi wa Jamii kupitia mpango wa pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Kusini mwa New Hampshire nchini Marekani.
Ilipofika mwaka 2000 aliamua kujiunga na siasa ambapo aliteuliwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Mbunge wa viti Maalum katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kisha kuteuliwa kuwa Waziri wa Utalii na Biashara katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alichaguliwa mnamo mwaka 2005 kuwa Mbunge wa viti maalum na aliteuliwa tena kuwa waziri katika wizara ya kazi, jinsia na watoto.
Mwaka 2010 aligombea Ubunge wa jimbo la Makunduchi mkoa wa Kusini Unguja na kupata ushindi wa asilima 80.
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Jakaya Kikwete alimteua Mama Samia Suluhu Hassan kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia Muungano.
Nyota yake kisiasa ilizidi kung’ara ambapo mwaka 2014, alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba iliyokuwa na jukumu la kuandaa katiba mpya ya nchi.
Julai 2015 Dkt John Magufuli alimteua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Baadaye alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke katika historia ya nchi baada ya ushindi wa Dkt Magufuli katika uchaguzi huo wa mwaka 2015.
Kutokana na utumishi wake mahiri, Dkt John Magufuli alimteua kwa mara nyingine Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2020.
Mama Samia Suluhu Hassan alifunga ndoa mwaka wa 1978, na Hafidh Ameir, ambapo wamejaaliwa kupata watoto wanne.