Wakazi wa kijiji cha Namatumbusi wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wameishukuru Serikali kwa kuwajengea zahanati ambayo imewarahisishia upatikanaji wa huduma za afya.
Wakazi hao wamesema hayo baada ya Mwenge wa Uhuru kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati hiyo na kuzindua mfumo wa GOT Homis katika kijiji chao.
Wamesema kwa muda mrefu walikuwa wakitembea umbali wa kilomita nane kufuata huduma za afya katika zahanati za jirani.
Ujenzi wa zahanati hiyo ya kijiji cha Namatumbusi umegharimu shilingi milioni 93, ambapo Serikali kuu imetoa shilingi milioni 61, halmashauri ya Nanyumbu shilingi milioni 21 na Wananchi wamechangia zaidi ya shilingi milioni tisa.
Wakazi hao wamesema.waliamua kuchangishana kiasi hicho cha fedha na kuanza ujenzi wa zahanati hiyo kutokana na adha kubwa wanayoipata katika kupata huduma za afya.
Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa zahanati hiyo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi amewapongeza wakazi wa kijiji hicho cha Namatumbusi kwa kushirikiana na Serikali kukamilsha ujenzi wa zahanati hiyo.
Amesema kukamilika kwa miradi ya maendeleo kwa wakati kutasaidia kutoa huduma bora kwa Wananchi na kuondoa malalamiko ya Wananchi dhidi ya Serikali.