Washiriki wa zoezi la Ushirikiano Imara waagwa

0
176

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda amewataka maafisa na askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), vyombo vya usalama pamoja na watumishi kutoka taasisi za Serikali watakaoshiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2024 linalotarajiwa kufanyika nchini Rwanda kuanzia Juni 08, 2024, kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kupeperusha vema bendera ya Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi wakati wa kukabidhi bendera ya Tanzania kwa vikundi vinavyoshiriki zoezi hilo, Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu Meja Jenerali Fadhil Nondo amesema mazoezi ya pamoja kwa vikundi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki yanalenga kujenga uwezo wa pamoja na utayari katika kukabiliana na ugaidi, majanga ya asili, uharamia na ulinzi wa amani.

Zoezi la Ushirikiano Imara linashirikisha vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na watumishi kutoka Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.