Wapuuzeni wanaopinga mpango wa vifurushi vya bima ya afya

0
325

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema kuwa wanaopinga utaratibu wa vifurushi vya bima ya afya hawawatakii mema watanzania.

Gambo ameyasema leo wakati akizindua mpango wa uhamasishaji wa wananchi kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupitia vifurushi vipya katika soko la Mbauda jijini Arusha.

“Ukisikia mtu anapinga mpango huu hakutakii mema kwani pindi unapopatwa na matatizo hatakuja kukusaidia hivyo tuwapuuze na tujiunge na mapango huu wa bima ya afya. Gharama za matibabu kwasasa ni kubwa sana, unaweza kwenda hospotali gharama za matibabu zikawa ni kubwa kuliko kifurushi cha bima ya afya, ndugu zangu tujiunge na mpango huu ili tuwe na uhakika wa matibabu wakati wowote, amesisitiza Gambo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Mama Anne Makinda amesisitizia wananchi juu ya kuweka kipaumbele katika suala zima la bima ya Afya ndani ya familia zao.

“Ukifanya kazi matumizi ya kwanza iwe afya yako, tusiweke rehani maisha yetu, hautaweza kuwa na maendeleo kama hauna uhakika wa huduma za matibabu,” amesema Mama Makinda.

Kutokana na umuhimu huo amewataka viongozi wa mkoa pamoja na viongozi wa dini kushirikiana kwa pamoja katika kuwahimiza na kuwakumbusha wananchi juu ya kuwa na bima ya afya.