Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amewapandisha vyeo maafisa wawili wa polisi mkoani Arusha wanaofanya kazi katika kituo cha polisi cha utalii na diplomasia, baada ya kutoa huduma bora kwa watalii.
Waliopandishwa vyeo ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi Waziri Tenga ambaye amepandishwa cheo na kuwa Mrakibu wa Polisi na Mkaguzi wa Polisi Anthony Mwaihoba ambaye amepandishwa cheo kuwa Mrakibu Msaidizi wa Polisi.
Mhandisi Masauni amesema amewapandisha vyeo askari hao baada ya kupokea barua kutoka ubalozi wa Tanzania nchini Italia iliyoandikwa na watalii raia wa nchi hiyo waliofika nchini hivi karibuni kwa ajili ya shughuli za utalii, wakiwapongeza polisi hao kwa kuwapatia huduma bora walipokuwa hapa nchini.
“Askari hao wamekua mfano bora wa kuigwa kwa kuitangaza nchi yetu vizuri Kimataifa hususani kipindi hiki ambacho Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anautangaza utalii kupitia filamu ya The Royal Tour”. amezema waziri Masauni