Wanawake watakiwa kutumia utamaduni kujipatia kipato

0
167

Wanawake nchini wametakiwa kuyatumia mazao ya utamaduni katika kujipatia kipato kwa kuwa mazao hayo ni sehemu ya vivutio vikubwa vya utalii wa kiutamaduni kwa watanzania.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja wakati wa uzinduzi wa onesho la Mchango wa Wanawake katika Utalii lililoandaliwa na Wanawake wa Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na wadau wengine katika Kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam.

Aidha Naibu waziri Masanja, licha ya kuipongeza Makumbusho ya Taifa kwa maadhimisho hayo yaliyobeba shughuli mbalimbali za wanawake na utalii, amesema ipo haja sasa ya jamii kuzitumia mila na desturi zetu katika kukuza utalii nchini na kuzitumia kama fursa za ajira.

Masanja ametoa wito kwa taasisi zinazojihusisha na utalii kuwashirikisha wanawake katika kazi zao na wanawake nao wasimame kidete katika kuhakikisha kuwa wanashiriki katika kuhamasisha na kutangaza utalii nchini kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.