Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Idadi ya watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA) Dkt. Wilfred Ochan, amewahimiza wanawake kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la Sensa ya watu na makazi litakalofanyika Agosti mwaka huu.
Ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam katika warsha ya siku moja ya mafunzo maalumu kwa wanahabari yaliyoandaliwa na UNFPA kwa lengo la kuwajengea uelewa Wanahabari kuhusu zoezi la sensa la mwaka huu na kufafanua kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika jamii hivyo wanapaswa kutumiwa ipasavyo katika kufikisha ujumbe wa sensa kwa jamii.
“Kila mwaka ifikapo Machi 8, Umoja wa Mataifa ,Serikali na wadau wa maendeleo ya kijinsia tunaadhimisha siku hiyo ambayo kwa mwaka huu kauli mbiu yake ni “Usawa wa Kijinsia wa Leo kwa kesho endelevu”, kwa Tanzania kauli mbiu ni kizazi cha haki na usawa kwa maendeleo endelevu,tujitokeze kuhesabiwa” amesema Dkt. Wilfred Ochan.
Ameongeza kuwa, kuelekea siku ya wanawake Duniani lengo la maendeleo endelevu SDGs namba 5 limelenga kufanikisha usawa kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana kwa kutambua na kuthamini mchango wa wanawake na kazi zao majumbani kupitia mgawanyo wa majukumu ya kijamii miundombinu na sera za kutetea jamii na kupata mgawanyo sawa wa majukumu katika familia na ngazi ya Taifa.
Naye Afisa Mawasiliano wa UNFPA amewasihi Waandshiwa habari kutoa elimu na kuwahimiza wanchi kujitokeza katika zoezi la Sensa litakapowadia kwani ni wajibu na haki kwa katika mstakabali wa maendeleo ya Jamii na Serikali.