Wajasiriamali mkoani Kigoma wametakiwa kuzitumia taasisi za kifedha kupata taarifa mbalimbali za mikopo, kutunza akiba pamoja na kufahamu namna ya kutunza kumbukumbu ili waweze kuendeleza biashara zao na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika wilaya za Bihigwe na Kigoma, Meneja wa CRDB kanda ya magharibi, Said Pamui amesema ni muhimu kwa wajasiriamali kuwa na mpango maalum wa utendaji utakaochochewa na utunzaji wa kumbukumbu za matumizi sahihi ya fedha kwa kuzingatia vpaumbele vya maendeleo.
Semina hiyo ambayo imewakutanisha wajasiriamali wanawake kwa nyakati tofauti katika wilaya ya Buhigwe pamoja na Manispaa ya Kigoma ujiji imekuwa na manufaa makubwa ambapo baadhi ya wajasiliamali wamesema mpango huo utakuwa na msaada kwao ikiwemo kuepukana na changamoto ya ukosefu wa mitaji, utunzani wa kumbukumbu na utafutaji wa masoko.
Pamui akaongeza kuwa, “Benki ya CRDB inaamini kwamba kumjuza na kumuelekeza mwanamke katika fani mbalimbali za ujasiliamali itakuwa imefanikiwa kuliendeleza Taifa kwa kiwango kikubwa kiuchumi.’’
Mkuu wa kitengo cha uwezeshaji wanawake kiuchumi CRDB, Rachel Senni amesema lengo ni kumuinua mwanamke kiuchumi kwa kumpatia elimu ya kupata mikopo, kutunza akiba pamoja na kufahamu namna ya kutunza kumbukumbu ambapo akaunti ya malkia imeelezwa kuwa suluhisho la changamoto kwa wajasiliamali wanawake.