Wanaume wa wilaya ya Kibondo wavunja ukimya juu ya manyanyaso

0
1158

Baadhi ya wanaume katika kata ya Kibondo mjini wilayani Kibondo mkoani Kigoma wamelalamikia vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia wanavyofanyiwa na wake zao ikiwemo kupigwa pamoja na kufanyishwa kazi za ndani.

Licha ya kutendewa vitendo hivyo,wanaume hao wamesema kuwa wanashindwa kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wanaotendewa na wake zao kutokana na changamoto zao kutotatuliwa.

Baadhi ya wanaume hao wamesema wameamua kuvunja ukimya kuhusu vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi yao ili wapate msaada na kuondokana na vitendo hivyo.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kata ya KIBONDO Mjini Phinias Samizi amesema wanawake na watoto ndio wahanga wakubwa wa unyanyasaji wa kijinsia katika kata hiyo hivyo taarifa hiyo kutoka kwa wanaume hao wanaipokea na wataifanyia kazi.

Hayo yamebainika katika Mdahalo uliolenga kuielimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa kijinsia ambao umeendeshwa na shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la kivulini.