Wanasheria wa serikali wakutana Dodoma

0
2458

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amewataka wanasheria wa serikali kuhakikisha sheria wanazozisimamia zinakidhi matarajio ya maendeleo na ustawi wa wananchi maskini.

Jaji Mkuu ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wanasheria walio katika utumishi wa umma unaofanyika jijini Dodoma, mkutano unaowakutanisha wanasheria 900 kutoka wizara mbalimbali, idara , taasisi za serikali na mamlaka za serikali za mitaa.

Akitilia mkazo sheria zinazolenga kuwasaidia wananchi maskini, Jaji Mkuu amesema kuwa sheria hizo ni lazima ziwasaidie kunufaika na Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo ni pamoja na Watanzania kuishi maisha yanayolingana na uchumi wa kati na kujenga utawala bora.

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma pia amewataka wanasheria hao wa serikali kuhakikisha kuwa ubora wa huduma za kisheria wanazozitoa zinakidhi mahitaji ya uchumi wa kati na kutumia ujuzi, weledi na uadilifu wao katika kutoa ushauri kwa maslahi ya Taifa.

Ametahadharisha kuwa ikiwa wanasheria hao watashindwa kutumia ujuzi wao, weledi na uadilifu katika kutoa ushauri wa kisheria wanaweza kusababisha mkanganyiko miongoni mwa jamii ya Watanzania.
Baadhi ya mada zitakazowasilishwa katika mkutano huo ni nafasi na majukmu ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itayotolewa na Mwanasheria Mkuu wa serikali Dkt Adelardus Kilangi, nafasi na majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na nafasi na majukumu ya ofisi ya Taifa ya Mashtaka.