Wanaovujisha mitihani waonywa

0
2057

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaonya maafisa elimu na walimu kutojihusisha na vitendo vya wizi wa mitihani vinavyofanywa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kwa kuwa vinawadharirisha.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa onyo hilo baada ya kukabidhiwa vyumba vya madarasa vya shule za msingi Nyakato na Kashozi wilayani Bukoba mkoani Kagera, vyumba vilivyojengwa kwa msaada wa serikali ya Japan baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi mwaka 2016.

“Kama kweli umemuandaa mtoto huna sababu ya kuiba mitihani na mtoto hawezi kufikiria kuiba mitihani kwa sababu yuko nje ya mfumo,  Walimu heshimuni maadili ya kazi ya ualimu”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Amesema kuwa  tathmini ya elimu katika shule za msingi na sekondari hufanyika kwa kufanya mitihani, hivyo ametaka dosari ya udanganyifu wa mitihani iliyojitokeza katika mitihani ya darasa la saba mwaka huu isijirudie tena.

Hivi karibuni Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) lilifuta matokeo ya mtihani ya darasa la saba kwa shule za msingi zote za halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuvujisha mitihani.