Wanaotuhumiwa kumuua mtendaji wa mtaa wanaswa

0
107

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya afisa mtendaji wa Serikali ya mtaa wa Mbezi Msumi, Kelvin Mowo  (38) mkazi wa Bunju mkoani Dar es Salaam.
 
Kamanda wa polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Muliro Jumanne amesema tukio hilo limetokea tarehe 11 mwezi huu majira ya asubuhi katika eneo la Mbezi Msumi  wilayani Ubungo,  katika ofisi za Serikali ya Mtaa ambapo marehemu alikuwa akisikiliza mgogoro wa ardhi.
 
Amesema wakati Kelvin akiendelea na majukumu yake ghafla watu hao waliingia ofisini na mmoja akatoa panga na kumshambulia, kitendo kilichosababisha apate majeraha makubwa na alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitalini.
 
Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, majina ya watuhumiwa hao yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi na kwamba upelelezi huo ukikamilika watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo.