Wanaolisha zaidi ya watu 300 kutumia nishati mbadala

0
263

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba amesema kuwa serikali inaandaa kanuni zitakazozilazimisha taasisi za umma na binafsi zinazolisha zaidi ya watu Mia Tatu kwa siku kutumia nishati mbadala au kupanda misitu yao kwa ajili ya kuni na mkaa.

Waziri Makamba ametoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Hata hivyo Waziri Makamba amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa elimu kwa taasisi na watu mbalimbali ili kuhakikisha matumizi ya mkaa na kuni yanapungua, lengo likiwa ni kuzuia uharibifu wa mazingira.

Kuhusu suala la Muungano, Waziri Makamba amewataka Watanzania kutokubali kufarakanishwa na  kutenganishwa kwa sababu ya changamoto  zilizopo na kwamba Ofisi yake itaendelea kuzitatua changamoto zote pindi zinapojitokeza.

Waziri Makamba pia ameendelea kuhamaisha upandaji wa miti Milioni 1.5 katika kila halmashauri nchini, lengo likiwa ni kunusuru uharibifu wa mazingira.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis ameiomba serikali kulipa uzito suala la uhifadhi wa mazingira huku Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Latifah Chande akiiomba serikali kuondoa kero za muungano.

Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeomba kupatiwa takribani Shilingi Bilioni 29 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ili iweze kukamilisha shughuli zake mbalimbali.