Utafiti mpya uliofanyika hivi karibuni umeonesha kuwa watu wenye umri wa miaka 50 na zaidi wanaolala kwa saa tano au chini ya hapo wapo hatarini kupata magonjwa sugu ikilinganishwa na wale wanaopata muda zaidi wa kulala.
Utafiti huo uliochapishwa Oktoba 18 mwaka huu katika jarida la PLOS Medicine uliangazia takribani watu 8,000 nchini Uingereza ambao hawakuwa na ugonjwa sugu wakiwa na miaka 50.
Wanasayansi waliwataka washiriki hao kutoa taarifa za muda ambao wanalala kwa kila miaka minne au mitano kwa kipindi cha miaka 25.
Watu waliofuatiliwa ambao walilala kwa saa 5 au chini ya hapo walikuwa katika hatari kwa 30% zaidi ya kupata magonjwa hayo kuliko waliokuwa wakilala kwa walau saa 7.
Waliofikisha umri wa miaka 60, hatari iliongezeka hadi 32%, miaka 70 ikafika 40%.
Magonjwa hayo ni pamoja kisukari, saratani, ugonjwa wa moyo, kiharusi, moyo kushindwa kufanya kazi, ugonjwa wa mapafu, magonjwa ya figo, magonjwa ya ini, sonona, tatizo la akili na mengine mengi.
Aidha, utafiti mwingine umeonesha vijana wasiolala vya kutosha usiku, kwa saa 7 hadi 9 wako hatarini pia kupata magonjwa sugu kama vile kiribatumbo na shinikizo la juu la damu, kwa mujibu wa idara ya kudhibiti magonjwa ya Marekani.