Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ametangaza vita dhidi ya wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ghali tofauti na bei elekezi.
Makonda amesema ifikapo kesho, Mei 4, 2020, kikosi kazi kitafanya ukaguzi na watakaobainika kuuza bidhaa hiyo kwa bei ya juu watakamatwa na serikali itataifisha sukari yao.
Hatua hiyo imekuja baada ya kiongozi huyo kubaini uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wanaouza sukari kwa bei ya hadi TZS 4,500 kinyume na bei elekezi ya serikali ya TZS 2,600, jambo linalopelekea maumivu na gharama kwa wananchi.
Makonda amewaelekeza wakuu wa wilaya zote tano za Dat es Salaam kuhakikisha msako huo unaanza na asisalie mfanyabiashara yeyote anayeuza sukari kwa bei ya isiyo sahihi.