Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza kuondolewa kazini kwa Meneja wa TEHAMA wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wasaidizi wake, hadi hapo uchunguzi zaidi utakapokamilika.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo mkoani Dar es salaam kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao chake na Menejementi pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo ikiwa ni siku moja tu baada ya Dkt. Kalemani kuwasimamisha kazi kwa muda wa siku 10 Meneja huyo wa TEHAMA wa TANESCO na Wasaidizi wake wawili kufuatia kutokea kwa hitilafu katika mfumo wa kununua umeme wa LUKU kwa njia ya kielektroniki, hali ikiyosababishwa adha kubwa kwa watumiaji wa huduma hiyo kwa siku kadhaa.
“lazima tufundishane kuwa makini, kila siku lazima tukague vifaa vyetu ili huduma ipatikane muda wote. Hakuna kuwasimamisha kwa siku 10, wakae pembeni hadi timu inayochunguza itakapotoa matokeo. Inawezekana sio wao tu, Waziri endelea na uchunguzi,” ameagiza Waziri Mkuu Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa ameiagiza TANESCO kuhakikisha inakuwa na mfumo wa dharura ‘backup’ utakaotumika pindi kunapotokea changamoto za kimfumo.
“Mmetengeneza usumbufu mkubwa sana, mlijua lazima kuwe na backup lakini hakuna, toka pale tulipoanza kutoa huduma mpaka leo kwanini hakuna backup, hilo ni jukumu lenu,” amesema Waziri Mkuu.