Wanaoficha kemikali ya kuchenjulia madini waonywa

0
193

Serikali kupitia Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba imesema itachukua hatua kali za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya vibali vyote na kuwafikisha mahakamani wale wote watakaobainika kuficha kemikali za kuchenjulia madini aina ya cyanide na baruti hali inayokwamisha shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini kuendelea
 
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo Desemba 19, 2022 mjini Morogoro kwenye mkutano wa wakaguzi wa migodi na baruti nchini wenye lengo la kupeana uzoefu kwenye ukaguzi na usimamizi wa masuala ya afya, mazingira kwenye shughuli za uchimbaji wa madini kama moja ya mikakati ya kupunguza ajali na kuwa na uchimbaji endelevu usioathiri mazingira.
 
Amesema, Serikali imeweka mikakati ya kutosha ikiwa ni pamoja na kukutana na wasambazaji wa kemikali za cyanide kwa ajili ya kupata maoni ya namna bora ya upatikanaji wa kemikali hizo kwa bei ambayo ni nafuu ili wachimbaji wa madini hususani wadogo waweze kunufaika huku Serikali ikipata kodi stahiki.
 
Akizungumzia mikakati ya Serikali kupitia Tume ya Madini katika kupunguza ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, Mhandisi Samamba amesema tangu kuanzishwa kwa Tume ya Madini ajali kwenye shughuli za uchimbaji wa madini zimeendelea kupungua kutokana na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na wataalam kutoka Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini.