Wananchi watakiwa kuhakiki usajili wa laini

0
268

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya uhakiki wa laini za simu kwa lengo la kutambua laini zilizosajiliwa kwa majina yao ili kuepuka kuhusishwa na makosa ya utapeli mitandaoni.

Amesema kuwa ni muhimu kwa kila mwananchi kuepuka kusajili laini kwa kuweka alama ya kidole zaidi ya mara moja ili kuzuia usajili wa laini nyingine za ziada ambazo zinaweza kutumika kufanya uhalifu mitandaoni

“Wananchi wengi wamekuwa wahanga wa utapeli mitandaoni hivyo wizara imejipanga kuimarisha mifumo ya kulinda faragha na taarifa binafsi ili zisitumike vibaya na watu wasiokuwa na nia njema,” alizungumza Dkt. Ndugulile

Aidha, amewaasa wananchi kuacha kutoa taarifa binafsi au kufuata maelekezo yeyote kwa watu wanaopiga simu na kujitambulisha wanatoka dawati la huduma kwa mteja katika makampuni ya simu ili kuepuka kutapeliwa

Ameongeza kuwa namba wanayotakiwa kupigiwa na makampuni ya simu ni namba 100 na sio kupigiwa na namba kutoka mitandao tofauti na mitandao wanayotumia huku wakijitambulisha wametoka huduma kwamteja na kuomba taarifa zao za kifedha au kutaka kujua salio lililopo katika laini zao za simu.