Wananchi wamuomba DC Jokate Mwegelo kusimamia ujenzi wa msikiti

0
525

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo amewahakikishia waumini wa dini ya Kiislaamu wilayani hapo kwamba watashirikiana bega kwa bega kujenga msikiti mkubwa wa kisasa wa ghorofa mbili.

Hatua hiyo ya ujenzi wa Msikiti wa Wilaya ya Kisarawe ambao unatarajia kugharimu shilingi milioni 500 hadi kukamilika kwake unalenga kuondoa changamoto kubwa ya ufinyu wa eneo la kufanyia ibada inayowakabili waumini wilayani Kisarawe.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ujenzi wa msikiti huo Jokate Mwegelo amewahakikishia waumini wa dini hiyo kwamba uhakika wa kukamilika kwa ujenzi huo utakamilika kwa wakati na tayari na ameshaanza kuzungumza na wadau wa ndani na nje kusaidia ujenzi huo huku akitoa rai kwa Watanzania kutoa sadaka kwa ajili ya ujenzi huo wa msikiti mkubwa na wa kisasa.

Amesisitiza msikiti huo ndio utakaobeba taaswira ya misikiti mingine ya Wilaya hiyo ambapo amesema kuna mambo mengi makubwa ambayo wananchi wa Kisarawe wamefanya, hivyo na ujenzi wa msikiti huo wa kisasa nao utawezekana.

Jokate ambaye pia amepewa nafasi ya ulezi wa msikiti huo amesema suala la kutoa ni la kila muumini hivyo kwa nafasi aliyopewa ni wazi kuwa inakwenda kuwa chachu ya kuongeza kasi ya ujenzi wenye ghorofa mbili ambao kiu yake kubwa kuona unakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.