Wananchi vijijini wahamizwa kuchangamkia fursa ya umeme

0
390
Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyonge

Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyonge amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali katika wilaya hiyo kuunga mkono na kuendeleza jitihada zinazofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) za kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa vijijini waliofikiwa na miundombinu ya umeme, kuchangamkia fursa kwa kuunganisha nishati hiyo na kuitumia kujiletea maendeleo.

Akizungumza na timu maalumu kutoka REA na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO)
Kaminyonge amesema,”Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametafuta fedha kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake katika sekta mbalimbali pamoja na sekta hii ya umeme. Ni lazima tumuunge mkono kwa hichi anachokifanya kwa kuhakikisha wananchi wanaelimishwa na kuunganisha umeme.”

Kwa mujibu wa Kaminyonge, Wilaya ya Maswa ina vijiji 120 na mpaka mwaka 2022 vijiji 29 pekee ndio vilikuwa havijafikiwa na miundombinu ya umeme na Rais alitoa zaidi ya shilingi Bilioni 5 kwa ajili ya kuhakikisha vijiji 29 vilivyobaki vinapata umeme mwaka huu 2023.

Msimamizi Miradi wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale

Msimamizi Miradi wa REA Kanda ya Ziwa, Mhandisi Ernest Makale amesema azma ya Serikali siyo tu kuwafikishia nishati bora wananchi wa vijijini bali pia kuhakikisha wanazitumia kwa lengo la kuboresha maisha yao na ya Taifa kwa ujumla.

Dadu John kijana kutoka Kijiji cha Mbaragane amewahamasisha vijana wenzake kuchangamkia fursa zitokanazo na uwepo umeme katika vijiji vyao kama alivyofanya yeye kwa kufungua saluni ya kiume ya kunyoa badala ya kukaa tu vijiweni.