Wananchi Kata ya Kinyerezi waunganishiwa mawasiliano

0
210

Wananchi wa Kifuru Kata ya Kinyerezi manispaa ya Ilala wameipongeza serikali kurejesha mawasiliano ya barabara kwa kujenga madaraja ambayo yalibomolewa na mvua za masika na kuathiri wananchi.

Wakizungumza na Mwandishi wa TBC Online, viongozi na wananchi wa mitaa hiyo wamesema kukamilika kwa miundombinu hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo kwani walipata adha kubwa kipindi cha mvua hali iliyosababisha shughuli za kiuchumi na kijamii kudorora.

“Tunaishukuru sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan  kwa hatua hii ya kurejesha mawasiliano yaliyokuwa yamekatika kwenye kata yetu na kusabisha kila kitu kukwama lakini sasa shuguli zetu zitafanyika bila usumbufu wowote,” wamesema wananchi hao.

Kwa upande wake Meneja TARURA Manispaa ya Ilala, Mhandisi Silvester Chinengo amebanisha kuwa ujenzi wa daraja na kilometa mbili za barabara ya Kifuru kwa Masista umegharimu shilingi milioni 607.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Ng’wilabuzu Ludigija ameridhishwa na Ujenzi huo na kumtaka mkandarasi kumalizia ujenzi wa mitaro ili kuepusha uharibifu wa miundombinu hiyo nyakati za mvua.

Wilaya ya Ilala ni miongoni mwa halmashauri ambazo miundombinu yake kama barabara na madaraja ziliathiriwa na mvua hivyo kulazimu serikali kuchukua jitihada za kurejesha mawasiliano katika mitaa mbalimbali wilayani humo.