Wanahabari watakiwa kuepuka upotoshaji

0
318

Mkuu wa wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Sima amewashauri waandishi wa habari kuzingatia misingi ya kiuandishi na weledi katika kuhabarisha jamii juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali. Sima ameyasema hayo mkoani Kagera wakati akifungua semina ya waandishi wa habari mkoani Kagera iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhusu miradi inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ule wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima – Uganda hadi Chongoleani Tanga – Tanzania. Amesema Wananchi wanategemea kujua yanayoendelea nchini kupitia vyombo vya habari na endapo waandishi wa habari watapotosha habari zao watajenga chuki na taharuki kwa Wananchi dhidi ya Serikali. “Rais Samia Suluhu Hassan anaujua vizuri huu mradi na anaufuatilia kwa karibu hivyo nashukuru kwa kuandaliwa hii semina, naamini wanahabari mtauongelea vizuri mradi huu baada kujua mengi mazuri yatakayotokana na kukamilika kwa mradi huu ikiwemo kukuza uchumi na pato la Taifa”. ameongeza Sima