Wanafunzi wengine watekwa nyara

0
188

Watu wenye silaha wamevamia chuo kimoja katika jimbo la Kaduna nchini Nigeria, na kuteka nyara idadi kubwa ya Wanafunzi.

Uongozi wa jimbo hilo la Kaduna umesema kuwa, wengi wa Wanafunzi waliotekwa nyara ni wa Kike.

Mpaka sasa haijafahamika ni watu ama kikundi gani kilichofanya tukio hilo katika chuo hicho cha misitu, ambacho kipo karibu na chuo cha mafunzo ya kijeshi.

Kwa sasa uongozi wa chuo hicho unaendelea kufuatilia taarifa mbalimbali ili kufahamu ni Wanafunzi wangapi walikuwepo chuoni wakati tukio hilo linatokea.

Wazazi na Walezi wa Wanafunzi wanaosoma chuoni hapo wamepiga kambi katika maeneo ya kuzunguka chuoni hapo, kusubiri taarifa kuhusu walipo Watoto wao.

Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya watu kutekwa nyara nchini Nigeria, ambapo watekaji wamekuwa wakidai fedha ili waweze kuwaachia huru mateka, huku shule zikiwa ni walengwa wakubwa.

Takribani Wanafunzi 800  wametekwa nyara na watu wenye silaha tangu mwezi Desemba mwaka 2020 hadi sasa,  na baadaye kuachiliwa baada ya kufanyika kwa majadiliano na watekaji.