Wanafunzi wanusurika bweni likiteketea kwa moto

0
385

Wanafunzi 36 wa Shule ya Sekondari ya Seminari ya Wasichana ya Mtakatifu Joseph iliyoko Bugando jijini Mwanza wamenusurika kifo baada ya bweni moja lenye vyumba vitatu kuteketea kwa moto.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Mwanza, Ambwene Mwakitobe amesema uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo ulioteketeza mali zote za wanafunzi zikiwemo madaftari, magodoro pamoja na nguo.

Moto ulioteketeza bweni hilo umefanikiwa kuzimwa na jeshi la zimamoto na uokoaji ambalo linaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto huo.

Wanafunzi 32 kati ya 36 waliokumbwa na janga hilo wamepata mshtuko na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambapo 27 kati yao wameruhusiwa baada ya kupatiwa huduma ya kwanza huku watano wakilazwa kwa ajili ya matibabu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Nyamagana, Dkt Philis Nyimbi ametembelea shule hiyo na kutoa wito kwa jamii kuwasaidia wanafunzi walioathiriwa na janga la moto.

Hii ni mara ya pili moto kuteketeza bweni shuleni hapo ambapo tukio la kwanza lilitokea miaka 13 iliyopita.