Wanafunzi 150 wa Sudan wapokelewa Muhimbili

0
423

Wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum, Sudan wamehamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo Dar es Salaam, ili kukamilisha mwaka wao wa mwisho wa masomo.

Akiwakaribisha wanafunzi hao Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Mohamed Janabi amesema, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini Sudan yamesababisha kufungwa kwa vyuo na baadhi ya shughuli kusimama hivyo Wanafunzi hao kushindwa kuendelea na ratiba yao ya masomo.

Amesema Madaktari hao Wanafunzi watafanya mzunguko katika idara mbalimbali ikiwemo idara ya upasuaji chini ya usimamizi wa Madaktari bingwa ili kuhakikisha wanapata maarifa yanayotakiwa.

Profesa Janabi amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili itatoa fursa kwa Wataalamu hao kujifunza kama ambavyo inatoa kwa Wataalamu wengine wa ndani na nje ya nchi na hata baada ya kumaliza masomo kama watapenda kufanya mafunzo tarajali (Intenship), hospitali ya Muhimbili itawapa nafasi hiyo.

Kwa upande wao Wanafunzi hao kutoka Sudan ambao ni wa mwaka wa tano wamesema kuwa, wamefurahi kupata fursa ya kuendelea na masomo katika hospitali kubwa na yenye wataalamu wa kutosha, na ni imani yao watapata fursa nzuri ya kujifunza.