Watu 17, ambapo 14 ni wa familia moja, wamefariki dunia na wengine 12 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Magira Gereza, Tarafa ya Mombo wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amesema Ajali hiyo imehusisha gari aina ya Mitsubishi Fuso iliyoligonga gari aina ya Coaster iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu na abiria 26 ikitokea jijini Dar es Salaam kwenda Moshi kwa ajili ya mazishi.
Waliofariki kwenye ajali hiyo ni wanaume tisa, wanawake sita, watoto wawili mmoja wa kike na mmoja wa kiume.
Majeruhi 10 wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo kuendelea na matibabu na wawili wamebaki Hospitali ya Wilaya Magunga huku hali zao zikiendelea vizuri.
Mgumba amesema miili ya marehemu ipo katika Hospitali ya Wilaya Magunga, Korogwe.
Chanzo cha ajali ni kimeripotiwa kuwa ni uzembe wa dereva wa gari aina ya fuso kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na ndipo lilipogongana uso kwa uso na Coaster hiyo.