Wamiliki wa ‘drones’ waagizwa kuzisajili TCAA

0
467

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imewaagiza wamiliki wa ndege ndogo zisizo na rubani (drones) kuhakikisha ndege hizo zimesajiliwa ifikapo Agosti 28, 2020.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA imeeleza kuwa agizo hilo ni utekelezaji wa kanuni za kiusalama za kudhibiti matumizi ya ndege zisizo na rubani za mwaka 2018 na kuwa yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua za kisheria.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, mtu au kampuni inayotaka kumiliki ndege hizo inatakiwa kuomba kibali TCAA kabla ya kuingiza na kusajili. Aidha, wamiliki wanatakiwa kuomba kibali TCAA na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi na serikali za mitaa wakati wa matumizi.

TCAA imewaelekeza wamiliki wa ndege hizo kufika katika ofisi zao za kanda kwenye mikoa mbalimbali pamoja na makao makuu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya usajili.