Watu watano wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya Alice Mtokoma miaka 56, mkazi wa Kijiji cha Usalule Mkoani njombe.
Hukumu hiyo ya kesi namba 84 ya mwaka 2014 imetolewa na Jaji wa Mahakama kuu Firmin Matogolo baada ya watuhumiwa hao kukutwa na hatia ya kumuua Alice Mtokoma kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Matogolo amesema watuhumiwa hao wamekutwa na hatia ya mauaji hayo kinyume na kifungu cha sheria na 196 na 197 kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya 2019.
Wakili wa serikali Matiko Nyangelo amesema washtakiwa waliohukumiwa na adhabu hiyo ya kunyongwa hadi kufa ni James Msumule, Emmanuel Ngailo, Izack Ngailo, Anitha Mbwilo na Upendo Mligo.
Chanzo cha mauaji hayo kimetajwa kuwa ni wivu wa mapenzi na imani za kishirikina.