Walioshindwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali kikaangoni

0
209

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameuagiza uongozi wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutafuta chanzo cha viongozi 52 kushindwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa wakati, na kuwachukulia hatua za kisheria.

Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kikwajuni jijini Zanzibar.

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 jumla ya Viongozi 2,578 walichukua fomu za tamko la rasilimali na madeni, ambapo Viongozi 2,556 walirejesha fomu hizo kwa wakati huku 52 wakirejesha fomu hizo nje ya muda uliowekwa.

Amesema Viongozi waliorejesha fomu hizo nje ya muda uliowekwa ni aina ya Viongozi wanaopewa kazi na kuacha kuzifanya, na pale inapotokea wakafanya hukamilisha kwa wakati wanaopenda wao.

Dkt. Mwinyi amewakumbusha Viongozi wote wa Umma waliotajwa katika sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhakikisha wanarejesha fomu hizo baada ya kuzijaza sio zaidi ya tarehe 31 Disemba 2021.