Waliosababisha madhara ya chanjo kwa mifugo wasakwa

0
178

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameagiza kutafutwa kwa wataalamu wa mifugo waliotoa chanjo ya mifugo katika kijiji cha Mlazo wilayani Chamwino mkoani Dodoma, na kusababisha baadhi ya mifugo kufa na mingine kupata madhara.

Waziri Ndaki ametoa agizo hilo alipofika katika kijiji hicho mara baada ya kupatiwa taarifa juu ya madhara yaliyojitokeza baada ya mifugo kupatiwa chanjo ya homa ya mapafu (CBPP).

Amesema zoezi la chanjo ya mifugo dhidi ya magonjwa linaloendelea nchini lina lengo zuri, lakini amesikitishwa na zoezi lililofanywa katika kijiji hicho cha Mlazo kwa kuwa halikufanywa kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu.

Pia Waziri Ndaki ameagiza kampuni ya Agristeps Limited iliyoingia mkataba na halmashauri ya wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kusimamia zoezi la utoaji chanjo, kuzuiwa kuendelea kutoa chanjo katika wilaya hiyo na kufikishwa kwenye kwa Baraza la Veterinari Tanzania kwa ajili ya uchunguzi.

Amezitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha watoa huduma walioingia nao mikataba ya utoaji chanjo za mifugo wanafuata taratibu za utoaji wa chanjo.

Kuhusu mifugo inayopata madhara na mingine kufa wakati wa utoaji chanjo, Waziri Ndaki amesema kuna haja ya kubadilisha sheria ya Veterinari ya mwaka 2003 na Sheria ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003, ili endapo mifugo itapata madhara mfugaji afidiwe.