Waliopoteza milioni 900 za Wastafuu ‘kuzitapika’

0
189

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma kuwashikilia viongozi wa vyama viwili vya ushirika vya walimu, Kurugenzi Saccos na Teachers Saccos kwa tuhuma za upotevu wa fedha za michango ya walimu wilayani humo zaidi ya shilingu milioni 900.

Ndejembi pia ametoa maagizo kwa wakurugenzi wa halmashauri za Mbinga Mji na Mbinga DC kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa ushirika wa halmashauri hizo kwa kushindwa kusimamia vyama hivyo kwa weledi na kupelekea kupata hasara ya fedha hizo.

Akizungumza na wastaafu wilayani humo Naibu Waziri Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan haitomvumilia mtu yeyote atakayejaribu kutumia fedha za wananchi katika kujinufaisha mwenyewe. Ameitaka TAKUKURU kuharakisha uchunguzi wa jambo hilo ili haki ya wastaafu hao iweze kupatikana.

“Haiwezekani wastaafu wetu hawa waliotumikia Taifa lao fedha zao ziliwe. Wazee wetu hawa walichangia fedha zao kwenye Saccos hizi wakitegemea wanapostaafu wapate fedha zao, sasa mnatuambia fedha hakuna zaidi ya shilingi milioni 900, jambo hili haliwezekani,” amesisitiza.

Amesema Kurugenzi Saccos wana deni ya shilingi milioni 500, Teachers Saccos wana deni la shilingi milioni 470, huku akiagiza pia na viongozi wa zamani pia wachukuliwe hatua maana ubadhirifu ulianzia kwao.