Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa mikoa na wilaya nchini kuhakikisha Wananchi waliokuwa wakiishi mabondeni ambao waliokolewa na kuhamishiwa kwenye maeneo salama hawarejei tena.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na Wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Kipindimbi wilaya ya Kilwa mkoani Lindi.
“Haikubaliki watu waliokuwa wakiishi mabondeni ambao kwa sasa wamehamishiwa kwenye maeneo salama kuona wamerejea tena mabondeni, Wakuu wa mikoa na wilaya hakikisheni Wananchi hao hawarudi mabondeni”, amesisitiza Waziri Mkuu.
Amesema Serikali inawataka Wananchi hao kutorudi tena mabondeni lengo likiwa ni kuwanusuru na maafa ya mafuriko yanayoweza kujirudia kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, Serikali inawajibika kuhakikisha Wananchi wote wanakuwa salama, hivyo ni vyema kuchukua hatua za kuwaondoa wote waishio mabondeni ili kuwaepusha na maafa yanayoweza kuwapata.
Mbali na kuzungumza na Wananchi katika kijiji hicho cha Kipindimbi, pia Waziri Mkuu ametembelea vijiji vingine vilivyokumbwa na maafa hayo ambavyo ni Nambilanje wilayani
Ruangwa, Nakiu na Njinjo wilayani Kilwa na Kitomanga kilichopo wilayani Lindi ili kujionea athari za mafuriko na kuwapa pole Wananchi.
“Naomba mpokee salamu za pole ninazozileta kwenu kutoka kwa Rais wetu mpendwa Dkt John Pombe Magufuli alizozitoa kwa Wananchi wote waliokumbwa na mafuriko hayo kwa kupoteza ndugu zetu wapendwa pamoja na mali”, amesema Waziri Mkuu.
Awali, mkuu wa mkoa wa Lindi, – Godfrey Zambi alisema kuwa mvua hizo zilizonyesha mfululizo zilisababisha maafa makubwa ambapo watu 21 walifariki dunia huku wengine 26,481 katika kaya 4,344 wakikosa makazi.
Amesema mbali na kusababisha vifo, pia maeneo mbalimbali ya kutolea huduma nayo yameathirika ikiwa ni pamoja na shule, zahanati, miundombinu ya barabara, maji na mashamba ambayo yamefunikwa na maji.
“Mvua hizi zilisambaa katika wilaya zote za mkoa wa Lindi, hata hivyo athari kubwa zilitokea kwenye wilaya za Kilwa kata zilizoathirika ni saba, Ruangwa kata 18, Liwale kata Tatu na Lindi kata Nne”, amefafanua Zambi.