Waliomuua Mtangazaji wa ITV wasakwa

0
235

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, – Ramadhan Kingai amesema makachero wa jeshi hilo wanaendelea na uchunguzi, na muda si mrefu watawafikia waliotekeleza mauaji ya Mtangazaji wa ITV, Blandina Sembu.

Kamanda Kingai amewaambia waandishi wa habari kuwa, kifo cha Blandina ni tukio la mauaji na kwamba Polisi walipata taarifa za mwili wa Mtangazaji huyo kutupwa mbele ya baa ya Maryland maeneo ya Mwenge saa tano usiku wa jana.

Amesema gari aina ya Toyota Noah ilifika katika eneo hilo na kusimama kwa muda mfupi kabla ya kuutupa mwili wa Blandina akiwa tayari amefariki dunia.

Kamanda Kingai ameeleza kuwa madereva wa bodaboda waliokuwa wamepaki jirani na eneo hilo walishuhudia gari lililowashaa taa likisimama katika eneo hilo na kisha wakaona mwili wa mwanamke umetupwa.

Kamanda Kingai amefafanua kuwa, uchunguzi wa awali umebaini Blandina hakuuliwa katika maeneo yale na kwamba mauaji yalifanyika sehemu nyingine, na pale wauaji walienda kutupa mwili wake.

Amesema, Blandina amekutwa na majeraha usoni.