Waliojiandikisha kuhama Ngorongoro waongezeka

0
203

Idadi ya wakazi wanajiandikisha kuhama kwa hiari kutoka katika hifadhi ya Ngorongoro inaendelea kuongezeka, huku awamu ya pili ya kuwahamisha wananchi walio tayari kuhama kwa hiari ikitarajiwa kuanza Alhamisi wiki hii.

Wananchi wa jamii ya Watatoga nao wamesema wapo tayari kuondoka katika kata ya Eyasi na kwenda kuishi Msomera mkoani Tanga, ili kupisha uhifadhi.

Diwani wa Viti maalum kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) Veronica Gitida amejitokeza kujiandikisha kuhama katika eneo hilo kwa hiari na kisha kuwataka wananchi wengine wajitokeze kuunga mkono jitihada za serikali za kulinda maeneo ya uhifadhi.

“Mimi ni kiongozi wa wananchi hapa, lakini nimekubali kuhama kwa hiari yangu kupisha shughuli za uhifadhi ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro.” amesema Veronica

Augustino Ginada ni Makamu Mwenyekiti Jamii ya Watatoga Tanzania, yeye anasema kuhama katika eneo la hifadhi ni jambo ambalo litawainua kimaendeleo, kwani wataweza kumiliki ardhi na nyumba za kisasa.

Awamu ya pili ya kuwahamisha wananchi wanaoishi katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro inatarajiwa kuanza Alhamisi wiki hii, ambapo kaya 24 zinatarajiwa kuhamia katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni mkoa wa Tanga.