Walioghushi vyeti kurejeshewa michango yao

0
231

Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti warejeshewe michango yao waliyochangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema watumishi hao ni wale walioondolewa katika utumishi wa umma wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti, lililoendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016 hadi Aprili mwaka 2017.

Katika zoezi hilo la uhakiki, zaidi ya watumishi elfu 14 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi na waliondolewa katika utumishi wa umma.

Serikali imeitaka mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSF kurejesha michango ya wafanyakazi hao iliyowasilishwa kwenye mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri.

Profesa Ndalichako ameweka wazi kuwa, michango ya watumishi hao itaanza kurejeshwa kuanzia Novemba Mosi mwaka huu na kwamba mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri wake akiwa na vielelezo kadhaa ambavyo atahitajika kuwa navyo.