Walimu nchini watakiwa kufanya kazi kwa umakini

0
1135

Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha amewataka waalimu wa somo la hisabati nchini kutokuwa chanzo cha wanafunzi kufanya vibaya katika somo hilo na badala yake wawe msaada kwa wanafunzi ili kuongeza ufaulu wa somo hilo na sayansi kwa ujumla.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo Wilayani Korogwe Mkoani Tanga wakati akifunga mafunzo kwa waalimu wa Somo la Hisabati kutoka katika halmashauri 12 nchini zilizofanya vibaya katika somo la hisabati katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne ambapo amesema baadhi ya waalimu wamekuwa wakichangia wanafunzi kulichukia somo la hisabati kwakuwa mbinu wanazotumia kufundishia sio shirikishi.

Jumla ya waalimu 48 wa somo la hisabati wa shule za msingi na sekondari kutoka Halmashauri 12 za Meatu, Mkalama, Simanjiro, Ukerewe, Gairo, Momba, Rufiji, Nyasa, Korogwe, Madaba, Ruangwa na Nanyamba ambazo zimefanya vibaya kwa miaka mitatu mfululizo katika matokeo ya darasa la saba na kidato cha nne wamepatiwa mafunzo ya kuwawezesha kupata ufaulu katika shule zao.