Walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa wapewa tuzo 400

0
595

Waziri Nchi-Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleimani Jafo amesema serikali ya awamu ya tano imejidhatiti kuendelea kutoa elimu bila malipo ili kupunguza watu wasiojua kusoma katika taifa.

Waziri Jafo ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akitunuku vyeti kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri katika mtihani wa taifa kidato cha nne na sita mwaka 2019-2020.

Mara baada ya kutunuku vyeti hivyo Waziri Jafo amebainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa elimu bila malipo nchini katika shule za sekondari na msingi umeongeza chachu ya ufaulu kwa wanafunzi.

“Serikali ya awamu ya tano imewekeza zadi ya shilingi trilioni 9 kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu bure ili kuharakisha maendelo ya uchumi wa kati.”

Aidha Waziri Jafo ametaka watendaji wa wizara ya elimu kuhakikisha wanafunzi wanaofanya vizuri kitaifa katika mitihani yao ya mwisho wanapewa fursa ya kuwa na chaguo wanalopenda sambamba na kupewa mikopo kwa asilimia 100 ili kuwasaidia kufikia ndoto zao.

Baadhi ya wanafunzi na walimu wameeleza kufurahishwa na uwekezaji uliofanywa na serikali katika uboreshaji wa elimu nchini hususani kwenye miundombinu na mazingira ya kusomea ambayo yamewachangia kufanya vizuri.

Zaidi ya tuzo 400 zimetolewa kwa wanafunzi na walimu waliofanya vizuri huku mwanafunzi aliyeshika nafasi ya kwanza kitaifa kutoka Kibaha Sekondari akiibuka na tuzo tano huku mwalimu bora kitaifa akitokea Shule ya Sekondari Kisimiri, wilayani Arumeru.