Walimu ‘kunolewa’ suala endelevu

0
347

Mratibu msaidizi wa Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari Tanzania (SEQUIP), Beatrice Mbigili, amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu wa shule za sekondari kama njia ya kuwajengea uwezo.

Ametaja mafunzo hayo kuwa ni mafunzo kazini kuhusu Mpango wa Shule Salama, mafunzo kazini kwa walimu wa Sayansi, Hisabati pamoja na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliono (TEHAMA) kwa walimu ili kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari nchini.

Beatrice ameongeza kuwa pamoja na kuwajengea walimu hao uwezo kwa njia ya mafunzo bado Serikali imeendelea na hatua nyingine zaidi ya kuhakikisha kila mwalimu anakuwa na kishikwambi na kuandaa mpango wa mafunzo ya namna ya kutumia vishikwambi hivyo pamoja kujenga maabara za Tehama katika shule zinazotoa masomo ya Tehama.

Sambamba na hilo amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya shule, ujenzi wa matundu ya vyoo, ujenzi wa maabara za Tenama pamoja na nyumba za walimu.

Akizungumza na walimu wa shule za Sekondari kutoka Mkoa wa Pwani na Mtwara katika semina ya programu ya shule salama, Beatrice amesema tafsiri halisi ya shule salama inaonekana pale ambapo kila mtoto anapata haki yake ya kielimu na ndio sababu serikali inaweka mazingira mazuri kuhakikisha njia za ufundishaji zimeimarishwa ili kuwafikia wanafunzi wote kupitia walimu wenye ujuzi na mbinu bora za kufundisha.

Mafunzo ya programu ya shule salama yanaendelea mkoani Lindi ambapo hii leo kundi jingine la walimu kutoka mkoa wa Mtwara na Pwani wamenza kupatiwa mafunzo yatakayodumu kwa siku tatu.