Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wanolewa

0
1883

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua mafunzo yanayoshirikisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini na kusema kuwa serikali inatarajia viongozi hao watasimamia nidhamu katika utumishi wa umma na wao wenyewe watakuwa kioo cha utumishi wa umma mara baada ya mafunzo hayo.

Akizungumza na viongozi hao mara baada ya kufungua mafunzo hayo jijini Dodoma, mafunzo yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi nchini, Waziri Mkuu Majaliwa amewaagiza Wakuu hao wa mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kuzingatia mipaka ya madaraka yao na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao zizingatie sheria, kanuni na taratibu za nchi.

“Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi ana mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi, nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu”, amesisitiza Waziri Mkuu.

Pia amewaagiza kusimamia suala la amani na utulivu kwenye mikoa yao ili wananchi waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote, kwa kuwa amani na utulivu ndiyo itaiwezesha nchi iendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Nchini, Profesa Joseph Semboja amesema  kuwa mafunzo hayo ya wiki moja yanazingatia maeneo makuu matatu ambayo ni pamoja na kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa jamii.