Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, -Gerald Kusaya ametoa wito kwa wakulima nchini kukata bima ya mazao itakayowahakikishia usalama katika shughuli zao.
Kusaya ametoa wito huo wilayani Mvomero mkoani Morogoro aliposhiriki zoezi la kutoa hundi ya shilingi milioni 23 kwa wakulima, ikiwa ni fidia baada ya mashamba yao ya mpunga kuharibiwa na mafuriko katika msimu uliopita wa kilimo, fidia iliyotolewa na Shirika la Bima la Taifa.
“Nimepewa taarifa kuwa msimu uliopita wakulima 32 kutoka wilaya tofauti kote nchini walikata bima kupitia Shirika la Bima la Taifa na mashamba yao kukumbwa na majanga mbalimbali, na sasa tunawakabidhi fedha kama fidia kwa mujibu wa sheria na taratibu za shirika hili,” amesema Kusaya.