Serikali imeendelea kuwapa uhuru wakulima wa zao la mahindi nchini kwa kuuza mazao yao sehemu yoyote na kwa bei yoyote bila kuwekewa vikwazo kama ilivyo kwa mazao mengine ya chakula na biashara.
Hayo yamesemwa na Naibu Waaziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akizungumza na wakulima wa matunda ya parachichi na mahindi mjini Njombe ambapo ameongeza kuwa hakuna kiongozi wa serikali atakayempangia mkulima katika uuzaji wa mazao.
“Kama Naibu Waziri wa Kilimo, debe la mahindi hata muuze elfu hamsini hakuna mtu atakayewaingilia katika kuuza mazao yenu. Ni lazima tuiheshimu sekta ya kilimo kama sekta nyingine zozote,” amesema Bashe.
Aidha, Bashe amewataka wananchi watakaoshindwa kutumia unga wa mahindi kwa sababu ya gharama wawe huru kununua zao jingine la chakula kama mchele au mihogo kuliko kumnyanyasa mkulima wa mahindi kwa kuingilia sekta ya kilimo huku akiwataka wakulima kuongeza uzalishaji.